Lewandowski Atupia Hat-trick Kuwarejesha Barcelona Kileleni

 
Robert Lewandowski amewarejesha Barcelona katika uongozi wa msimamo wa La Liga akifunga hat-trick ya kuvutia katika kipindi cha kwanza na kuipa Barcelona ushindi wa 3-0 dhidi ya Deportivo Alavés.

Real Madrid walishinda dhidi ya Villarreal mapema jana na kufanya wawe alama sawa na Barcelona, alama 21, kabla ya leo Barcelona kurejesha uongozi wao. Nyota wa mchezo wa leo kwenye Uwanja wa Mendizorroza alikuwa mshambuliaji hatari Lewandowski aliefungua akaunti ya mabao dakika ya saba tu ya mchezo. Mshambuliaji huyo kutoka Poland alipiga kichwa kutoka kwa krosi nzuri ya Raphinha, na kuwaweka Barca mbele mapema.

Lewandowski alifunga bao lake la pili dakika ya 22, akimalizia kwa karibu baada ya pasi nyingine nzuri kutoka kwa Raphinha. Alikamilisha hat-trick yake dakika 10 baadaye, kwa kupiga shuti lililomshinda kipa Antonio Sivera kufuatia pasi kutoka kwa Eric García. Hat-trick hiyo ya dakika 32 ilikuwa ya nne kwa kasi zaidi katika historia ya Barcelona kwenye La Liga.

Akiwa na mabao 12 katika mechi 11 kwenye mashindano yote msimu huu, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 anaendelea kuwa mkombozi mkubwa kwa vigogo hao wa Catalonia, ambao wana wastani wa zaidi ya mabao matatu kwa kila mchezo kwenye La Liga msimu huu.

“Tulicheza vizuri tangu mwanzo, na pasi nzuri zilifanya kazi yangu kuwa rahisi leo,” Lewandowski alisema baada ya mchezo. “Tulidhibiti mchezo, hasa katika kipindi cha pili, lakini bado kuna mambo ya kuboresha.”

Ushindi huu wa Barcelona unakuja baada ya kipigo cha kushtukiza walichokipata dhidi ya Osasuna wiki iliyopita, ukiwawezesha kuendelea kushikilia uongozi katika mbio za ubingwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post