Muujiza wa Instabul: Usiku wa Kihistoria Katika Soka

Leo ‘watoto wa 2000’ kaeni pembeni kidogo mtusikilize wakubwa wenu tuwasimulie kuhusu usiku maarufu katika soka, usiku uliojaa miujiza na uchawi, katika usiku ambao waingereza hawatokaa wausahau na waitaliano hawatotaka waukumbuke, usiku uliopewa jina Miracle of Istanbul yani Muujiza wa Instanbul, Kama wewe sio Mtoto wa 2000 lakini mpaka sasa hivi bado hujaelewa kuwa tunazungumia mchezo wa Fainali ya UEFA 2005 kati ya Liverpool na Ac Milan na wewe kaa nao nyuma kule usikilize kwa makini.

Vuta picha: ni jioni ya aina yake katika mji wa Istanbul, Uturuki, tarehe 25 May 2005, barabara hazipitiki na baa kama Ritim, U2 Istanbul Irish Pub haziingiliki watu wamejaa wanachapa ulabu. Upande wa Mashariki wa jiji hili la maraha, maeneo ya Basaksehir upatikanapo uwanja wa mpira wa nyota tano uitwao Atatürk Olympic Stadium hali ni tofauti. Kama kelele za viwanda, magari, na miziki katika vilabu zingesimama kwa muda ungeweza pia kusikia sauti za mapigo ya nyoyo za watu kwa kimuhemuhe cha kusubiri kwa hamu mchezo huu wa fainali ya UEFA ukiwakutanisha miamba hawa wawili kutoka Uingereza na Italia.

Atatürk Olympic Stadium

Upande mmoja kulikuwa na wababe Ac Milan. Wakiwa wameshwahi kubeba UEFA mara 6 katika mara zote 10 walizofika fainali ya UEFA, huku wakiwa na kikosi kilichosheheni wachezaji bora zaidi wa kipindi hicho kama vile nahodha Paolo Maldini, dimba la kati lilitawaliwa na fundi Andrea Pirlo, huku mtu mbaya Gennaro Gattuso akikimbiza winga ya kulia, pia walikuwa na Kaka, Seedorf na Shevshenko, kwa kifupi ni kwamba hii mechi ilikua imeisha kabla haijaisha, Ac Milan waliingia wakiwa ‘favourites’ huku upande wa Liverpool wakiongozwa na Steven Gerald, John Arne Riise, Xabi Alonso na Luis Garcia wao waliingia kama ‘underdogs’.

Muda ukafika, kila kitu kipo tayari, mashabiki wamekaa sehemu zao wakisubiri shughuli hii ya kiume ianze, pilato wa mchezo bwana Manuel Gonzalez anasubiriwa yeye tu kupuliza kipenga mambo yawe mambo!

Dakika ya kwanza tu Djimi Traore wa Liverpool akafanya kosa lililowagharimu Liverpool kwa kucheza faulo ambayo ikapigwa na mtaalamu wa hizo kazi ‘Andre Pirlo’ na nahodha Paolo Maldini akaiunganishia vizuri kambani. Dakika ya kwanza tu Ac Milan 1 Liverpools 0, haikushtusha Liverpool kufungwa, tu ilishangaza wameruhusu goli mapema hivyo tena katika mchezo muhimu kama ule.

Zimwi likujualo halikuli likakwisha, bahati mbaya sana kwa Liverpool Crespo alikua ni zimwi lisilowajua, hakuacha kipindi cha kwanza kiishe hajawafunga magoli mawili kufanya yawe ma 3 pamoja na lile moja la nahodha Maldini.

Mpaka mechi inaenda mapumziko Liverpool keshaoga goli zake 3 na amechezewa mpira mwingi, Liverpool walilowa na hawajanyeshewa na mvua. Sisi tusio na timu uwanjani yani Chelsea, Man U na Arsenal kazi yetu ilikuwa ni kula tu popcorn tukisubiri kipindi cha pili kianze mtu apigwe mkono au ikipendeza zaidi hata wiki sio mbaya si unajua tena adui muombee njaa? Hatukuwa na neno zaidi ya “tuliwaambia”

Kipindi cha Pili

‘Kwenye mpira wa miguu chochote kinaweza kutokea’ huu sio msemo tu. Usisherehekee kabla refa hajamaliza mpira, somo hili Ac Milan na sisi machawa wao tulijifunza vizuri ile siku.

Kocha wa Liverpool wakati huo, Rafa Benitez bado alikua anaamini katika kikosi chake. Aliamini wanaweza kufanya jambo usiku ule na mambo yakawaendea vizuri hivyo aliamua kufanya baadhi ya mabadiliko;

Kwanza anamtambulisha mchezoni Dietmar Hamman kubadili nafasi ya Steve Finnan, pia anabadili mfumo wa timu yake kucheza kutoka 4-4-1-1 kwenda 3-4-2-1 ili Riise na Smicer wacheze kwenye flanks, Hamman na Alonso wacheze dimba la kati huku nahodha Gerald akisaidia kupeleka mashambulizi mbele.

Mabadiliko hayo hayakuchukua muda kuwalipa kwani dakika chache baadae nahodha Steven Gerald aliwafungia Liverpool goli la kwanza kwa kichwa safi kabisa akiunganisha krosi ya Riise, huku Vladimir Smicer akiongeza goli la pili dakika mbili tu baadae kwa shuti kali mithiri ya kombola la masafa marefu na kumuacha Dida akilala yoo bila kuupata mpira huo.

Fainali sasa ikawa fainali, Ac Milan wanaongoza goli 3 kwa 2 huku wakiwa wanatamani kumwambia refa amalize mpira wao wanakaa mbali mana walikua wanapelekewa pumzi ya moto. Mashabiki wa Liverpool jukwaani wanaendelea kuimba muda wote, mashabiki wa Ac Milan wao walikuwa matumbo joto wasiamini kinachoendelea kutokea, huku sisi machawa tukikumbuka kwamba hatuna upande, yeyote atakaeshinda na ashinde, nani anapenda kukaa upande ambao damu zinatoka?

Kishapo maajabu yakaendelea kutokea, dakika tatu baadae Liverpool wakazawadiwa mkwaju wa penati baada ya Gattuso kumchezea madhambi Steven Gerald. Mchanganyiko wa hisia majukwaani, Liverpool shangwe nyingi huku Ac Milan wakiombea lolote litokee. Kipa wa Ac Milan, Mbrazili Dida alifanya kila aliloweza usiku ule ikiwa ni pamoja na kuokoa mkwaju huo wa penati uliopigwa na Alonso lakini isivyo bahati Alonso akakutana tena na mpira huo na kuutumbukiza nyavuni.

Mchezo Unamalizika Sare, Liverpool Anashinda Matuta

Hadithi ndefu fupi, pamoja na juhudi zote wanazofanya Ac Milan kurudi mchezoni, pamoja na msako wa kufa mtu wanaoufanya langoni mwa Liverpool ili kurudisha uongozi katika mchezo lakini bado Liverpool walikaza na dakika 90 zinamalizika kwa sare.

Dakika 30 za nyongeza zilikuwa chungu kwa timu zote mbili huku Liverpool wakishambuliwa zaidi. Rafael Benitez alikuwa na wakati mgumu usiku huu, nahodha Steven Gerald alifanya kila aliloweza na ungemkuta kila sehemu uwanjani akifanya kila jukumu isipokua kudaka tu kazi iliyokuwa ya Dudek ambaye alifanya kazi murua sana kuokoa michomo mingi langoni hususani shuti ya Shevshenko ambalo kapteni Gerald anakiri kwamba mkojo ulikaribia kumtoka akifikiri mpira huo umezama kimiani.

Dakika za 30 za nyongeza zilizojaa kila aina ya taabu, mateso, ‘unyanyswaji’ na pumzi ya moto zinakamilika pale Atatürk Olympic Stadium huku wakati huu shujaa akiwa kipa Jerzy Dedek ambaye anakua shujaa tena katika mikwaju ya penati na kuibeba Liverpool mabegani.

Siku zote anaelia mwishoni hadanganyi maumivu, analia kweli. Ac Milan walicheka kabla ya mechi, wakashangilia sana kipindi cha kwanza, lakini mwisho walilia kilio kikuu!

Ni miaka zaidi ya 18 sasa, lakini mpaka leo Dida bado hajawahi kuelewa ni nini kilitokea pale Atatürk Stadium, yani bado anauliza “nyie Liverpool mmepigaje hapo?”

Dida akiwa haamini kilichotokea

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post