Celtic Waichapa Chelsea Mabao 4-1 Katika Mechi ya Kirafiki

 

Klabu ya Celtic imefanikiwa kuwafunga Chelsea mabao 4-1 kwenye mchezo wa kirafiki uliochezwa hapo jana katika uwanja wa Notre Dame. Matokeo hayo yamekuwa ishara mbaya kwa kocha mpya wa Chelsea, Enzo Maresca, anapojitahidi kujenga upya klabu hii ya London.

Timu ya Celtic iliyo chini ya kocha Brendan Rodgers ilikuwa katika kiwango cha juu, ikidhibiti mpira na kupata nafasi nyingi za kufunga. Matt O’Riley ndiye alieanzisha safari hiyo ya msiba kwa Chelsea, akitoa pasi ya mwisho kwa Kyogo Furuhashi kufunga bao la kwanza kabla ya kuja kufunga tena yeye mwenyewe. Mabingwa wa Scotland waliongeza mabao mawili zaidi katika kipindi cha pili kupitia kwa Luis Palma, wakiwaacha Chelsea katika hali ya mshtuko.

Chelsea walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Christopher Nkunku kupitia mkwaju wa penalti. The Blues walipambana kuzuia mashambulizi huku wakionekana kukosa uelewano katika safu ya ushambuliaji, na kuonyesha kazi kubwa inayomsubiri Maresca katika kuijenga upya klabu hiyo.

Matokeo hayo bila shaka yataibua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wa Chelsea, ambao walikuwa wanatarajia mwanzo mzuri wa maandalizi ya msimu.

Mchezo huo ulionyesha tofauti kubwa kati ya timu hizo mbili, na Celtic wakionyesha kiwango kizuri katika utengenezaji wa nafasi, ufanisi wa kuzitumia na ubora katika kujilinda.

Post a Comment

Previous Post Next Post