Copa America 2024: Lionel Messi Akosa Penati, Argentina Yasonga Mbele

Timu ya taifa ya Argentina imefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Euro 2024 baada ya kushinda katika changamoto ya mikwaju ya penati kwa jumla ya penati 4 dhidi ya 2 za Ecuador katika mechi iliyochezwa alfajiri ya leo.

Nyota wa timu hiyo, Lionel Messi alirejea katika kikosi cha Argentina mara baada ya kukosa mechi ya mwisho ya hatua ya makundi kati ya Argentina dhidi ya Peru akiuguza jeraha la mguu na alifanikiwa kupiga kona iliyowawezesha Argentina kupata goli la uongozi kupitia kwa Lisandro Martinez.

Lionel Messi

Goli la Argentina lilidumu mpaka dakika za mwisho za kipindi cha pili ambapo Ecuador walisawazisha kupitia mkwaju wa penati hali iliyopelekea mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 1-1 hivyo kupelekea iamuliwe kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

Penati ya kwanza ya Argentina ilipigwa na Lionel Messi ambaye alijaribu kupiga kwa mtindo wa panenka lakini jaribio lake halikuzaa matunda kwani mpira huo uliishia kugonga mwamba wa juu wa goli la Ecuador.

Jaribio lililofeli la Messi halikuwakatisha tamaa Argentina ambao ni mabingwa watetezi wa mashindano hayo na pia Kombe la Dunia 2022.

Kwa mara nyingine tena, gokilipa wa Argentina Dibu Martinez aliokoa mikwaju miwili ya penati hivyo kuwaweka Argentina salama huku Julian Alvarez, Alexis Mac Allister, Gonzalo Montiel na Nicólas Otamendi wakifunga kwa upande wa Argentina hivyo kuwahakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali.

Akiongelea ushindi huo, kocha wa Argentina Lionel Scaloni amesema, “Kama timu, tuna imani na golikipa wetu. Hata kama Leo (Messi) alikosa kufunga bado tulijua kuwa kuna kitu kizuri kinaenda kutokea.”

Mpaka sasa Lionel Messi hajafanikiwa kufunga hata goli moja katika mashindano hayo huku akifanikiwa kutoa pasi moja iliyozaa goli katika michezo mitatu ya Copa America 2024 huku wakiwa wamebakiza mechi mbili (au moja kama wakiishia hatua ya nusu fainali) katika mashindano hayo.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post