Kombe la Dunia 1986: Goli la Mkono la Maradona

Diego Armando Maradona. Jina lenyewe tu linakutengenezea kichwani picha ya mchezaji mahiri wa soka, fundi wa kuucheza na kuuchezea mpira na mchezaji mwenye kasi uwanjani. Maradona alikuwa mchezaji wa aina yake, na huwezi kutaja wachezaji watatu bora wa muda wote ukaacha jina lake.

Diego Armando Maradona

Gwiji huyu wa soka, mzaliwa wa Argentina ana historia kubwa katika mchezo wa mpira wa miguu na kamwe dunia haitoacha kumkumbuka. Maradona anakumbukwa kwa kuwahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mashindano ya Kombe la Dunia la 1986, anakumbukwa pia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kuweka rekodi ya dunia ya uhamisho ghali zaidi: yani mwaka 1985 wakati Barcelona wanamsajili kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 5 ada hiyo ilikuwa ghali zaidi duniani, na hata mwaka 1984 Napoli wakimnunua kutoka Barcelona kwa pauni milioni 6.9 hali ilikua hiyohiyo.

Hatuwezi tukataja sifa na matukio muhimu ya mwamba huyu tukamaliza, itatuchukua muda mrefu kweli kweli. Lakini pia hatuwezi tukamaliza kumzungumzia bila kuitaja mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia ya mwaka 1986 ambapo Diego Maradona aliwaduwaza waingereza kwa magoli yake mawili yaliyowaondosha Uingereza katika mashindano kwa kipigo cha 2-1.

Goli la pili kufungwa na Maradona katika mechi hii, mwaka 2002 lilipewa heshima na UEFA na kutambulika kama goli bora la karne ya 20. Nyota huyo alifunga goli murua baada ya kuwanyanyasa vilivyo wachezaji wa Uingereza kwa vyenga na kamwe hawatokaa wasahau. Goli hilo tutaliongelea siku nyingine, hadithi yetu leo ni kuhusu lile goli la kwanza, goli maarufu ambalo yeye mwenyewe aliliita ‘Goli la Mkono wa Mungu’.

Kombe la Dunia 1982: Diego Maradona akikabiliana na Msitu wa Mabeki wa Ubelgiji 

Eneo la tukio ilikua ni uwanja wa Azteca Stadium huko Mexico City. Argentina wakiongozwa na nahodha Diego Maradona walikuwa wanakutana na Uingereza katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia na kila mmoja anataka kuisaidia timu yake iende hatua inayofuata.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huu kilimalizika kwa sare ya bila kufungana licha ya mechi kuwa na ushindani mkubwa. Kisha dakika ya 51 ya mchezo historia ikawekwa katika mpira wa miguu, japo sio kwa namna ambayo yeyote alitarajia.

Ulipigwa mpira mrefu kutoka eneo la katikati la uwanja kuelekea alipo Maradona ambaye alikuwa chini ya ulinzi mkali wa beki wa kati wa Uingereza, Steve Hodge. Kwa haraka sana Maradona akafikiria na kufanya kitu kisichotarajiwa, akaruka kichwa (sio kichwa pekee) kuuelekea mpira huo. Badala yake akatumia mkono kuupiga mpira uliomshinda golikipa wa Uingereza, Peter Shilton, na kuzama nyavuni.

Uwanja mzima ulikaa kimya kidogo, kisha ukaripuka kwa shangwe. Muamuzi wa mchezo, mtunisia Ali Bin Nasser, bila kujua amedanganywa akaita watu kati akiashiria kuwa lile ni goli.

Kama ambavyo alikuwa mahiri uwanjani, Maradona alikuwa mahiri katika kuongea pia. Baadae, baada ya mechi ile kuisha alisema kuwa eti ule ni “Mkono wa Mungu” uliopeleka mpira ule golini.

Wachezaji na mashabiki wa Uingereza walishikwa na hasira kali na mshtuko wasielewe kinachoendelea. Lakini yaliyotokea yalitokea, goli tayari lilishafungwa na refa akaruhusu. Lakini kama hiyo haitoshi, dakika 4 tu mbele Maradona akafanya tukio lingine lililowaacha midomo wazi. Anakokota mpira kutoka eneo lao (Argentina) wenyewe kwa kasi na kiufundi huku akiwapiga chenga wachezaji zaidi ya wa 5 wa Uingereza kabla hajaweka mpira kambani na kumuacha Shilton hajui la kufanya. Huwezi kutaja magoli bora kuwahi kufungwa duniani na usilitaje hili.

Ilikuwa ni mwaka 1986, na mechi ile iliisha kwa Argentina kushinda 2-1 wakifanikiwa kwenda hatua ya nusu fainali, lakini goli la “Mkono wa Mungu” bado ni goli maarufu duniani hadi leo!

Je, ilikua ni uhuni? Jambo la kawaida la kimchezo? Ushujaa? Au hali ya mchezaji kuamua kufanya lolote linalowezekana ili kuisaidia timu? Mjadala unaendelea hadi leo na utaendelea miaka nenda rudi.

Mpende au mchukie, lakini hauwezi kupinga kwamba magoli yote ya Maradona katika mechi hii dhidi ya Uingereza, la “Mkono wa Mungu” na lile Bora la Karne, yalimtengenezea nafasi kubwa na heshima katika historia ya mpira wa miguu.

Aendelee kupumzika kwa amani Diego ‘El Pibe de Oro’ Maradona, jina lake bado linaishi. Sisi tupo hapa kusimulia vizazi kuhusu yeye, hata siku tukiondoka maandishi haya yabaki na kutumika kama kielelezo cha ufundi wa soka wa gwiji huyu wa Argentina hivyo hatosahaulika kamwe. Adiós, hasta luego.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post