Mlinzi wa zamani wa Real Madrid na Manchester United, Raphael Varane, ametangaza kustaafu kucheza mpira wa miguu akiwa na umri wa miaka 31.
Varane, ambaye alijiunga na klabu ya Italia ya Como kwa uhamisho wa bure mwezi Julai, amefanya uamuzi huo baada ya kuumia goti kwenye mchezo wake wa kwanza na timu hiyo.
“Inatakiwa ujasiri mkubwa kusikiliza moyo wako na silika yako,” Varane aliandika kwenye Instagram. “Sijutii kitu, nisingebadilisha chochote.”
Mlinzi huyo wa Kifaransa amecheza soka kwa mafanikio makubwa sana na akishinda vikombe 18 na Real Madrid, ikiwa ni pamoja na mataji matatu ya La Liga na makombe manne ya Ligi ya Mabingwa. Pia alishinda Kombe la Dunia na Ufaransa mwaka 2018.
Sifa zimetiririka kwa Varane kutoka kwa wachezaji wenzake na maafisa wa soka. Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alimsifu Varane kwa kuwa “sauti muhimu katika msimamo wa kimataifa wa FIFA dhidi ya ubaguzi wa rangi.” Cristiano Ronaldo, ambaye alicheza na Varane wakiwa Real Madrid na Manchester United pia alimsifia nyota huyo.

Post a Comment