Eto’o Afungiwa na FIFA Mechi za Kimataifa kwa Utovu wa Nidhamu

 
Nyota wa zamani wa Barcelona na Chelsea, na sasa rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto’o amepigwa marufuku ya miezi sita kubudhuria mechi zozote za kimataifa zinazohusisha Cameroon. Marufuku hiyo ilitolewa na jopo la nidhamu la FIFA kufuatia ukiukaji wa sheria za shirika hilo la kimataifa wakati wa Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20.

FIFA haikueleza undani wa kilichotokea katika mchezo huo wa hatua ya 16 bora ambao Brazil walishinda dhidi ya Cameroon 3-1 baada ya muda wa ziada.

Eto’o alihukumiwa kuwa alivunja sheria za kinidhamu zinazohusiana na “tabia ya kukera na ukiukaji wa kanuni za mchezo wa soka” na utovu wa nidhamu wa wachezaji na maafisa, FIFA ilisema.

Marufuku hiyo inamzuia kuhudhuria mechi zozote za soka zinazohusisha timu za wanaume au wanawake za Cameroon, katika makundi yote ya umri.

Hii ni ya hivi karibuni katika mfululizo wa misukosuko inayomzunguka Eto’o tangu aingie madarakani kama rais wa FECAFOOT mwaka 2021. Mwezi Julai, alipigwa faini ya dola 200,000 na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa ukiukaji wa maadili unaohusiana na ushirikiano wake na kampuni ya kubashiri. Ingawa aliepuka tuhuma za upangaji wa matokeo, faini hiyo na marufuku ya hivi karibuni zimeibua maswali kuhusu uongozi wake.

Utawala wa Eto’o umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mzozo na Wizara ya Michezo ya taifa kuhusu uteuzi wa kocha wa timu ya taifa. Wakosoaji wake wamemtuhumu kwa tabia ya kidikteta na usimamizi mbaya wa FECAFOOT.

Post a Comment

Previous Post Next Post