Yanga na Azam Vita Bado Mbichi

Baada ya kukamilisha kumuondoa Azam Fc mshambuliaji Prince Dube, Yanga wapiga hodi tena mitaa ya Chamazi kumtaka kiungo Adolf Mtasingwa Bitegeko (24).

Adolf Mtasingwa (Katikati)

Mchezaji huyo tayari amewasiliana na mabosi wa Azam Fc akiwataka kuvunja mkataba wake uliobakiza miezi 6 tu kwa madai kuwa amepata timu nje ya nchi japo habari zinathibitisha kuwa tayari ana ofa mezani kutoka Yanga Sc.

Ikiwa mchezaji huyo nyota wa Timu ya Taifa ya Tanzania akikubaliwa kuvunja mkataba huo na viongozi wa Azam atatakiwa kulipa kiasi cha dola za kimarekani 300,000 kama takwa la kisheria la mkataba iwapo upande mmoja wa wanamkataba ukihitaji kuuvunja.

Wakati huohuo, inaripotiwa kuwa klabu ya Young Africans tayari imeanza mazungumzo na kiungo huyo ili kupata huduma yake msimu ujao. Azam wanao uamuzi wa kukubali kumuuza mchezaji huyo kwenye dirisha hili kubwa wapate kitika hicho cha pesa au wamkatalie aje kuondoka bure Januari mkataba wake utakapoisha!

Vitu muhimu vya kukumbuka katika suala hili la Mtasingwa ni kwamba; Mosi, bado ni mchezaji halali wa Azam na ana mkataba wa miezi 6 na matajiri hao na bado wanahitaji kumuongezea mkataba. Pili, Yanga wataweza kumsajili kama mchezaji huru katika dirisha dogo la mwezi Januari iwapo Azam wataendelea kumng'ang'ania na yeye akabaki na msimamo wa kutoongeza tena mkataba nao. Tatu, Azam hawataki kuwauzia Yanga mchezaji huyo!

Ikumbukwe kwamba, mwaka 2023 Azam Fc walikamilisha dili ya kumsajili Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka Yanga Sc mara baada ya Fei Toto kulipa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 100 kwa Yanga kuvunja mkataba nao. Habari za kuaminika zilidai kuwa pesa hiyo haikutolewa na Fei mwenyewe bali Azam ambao walihitaji huduma ya mchezaji huyo hali iliyozua mgogoro mkubwa hadi kupelekea Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati kuwaomba Yanga wamuachie Feisal akajitafute kwingine.

Ni kama vile Yanga bado walikuwa na kinyongo na sasa baada ya kufanikisha kumng'oa Prince Dube mikononi mwa Azam wanataka wamalizane na Adolf Mtasingwa.

Ikumbukwe pia kuwa klabu hiyo ya Azam mpaka sasa imeshawauza nyota wake tegemeo kama vile Kipre Junior alienunuliwa na mabingwa wa zamani wa Kombe la Shirikisho Afrika USM Alger, Prince Dube alieondoka baada ya kuvunja mkataba huku akitajwa kuelekea Yanga. Azam pia wameachana na Issa Ndala, Malickou Ndoye, Edward Manyama, Ayoub Lyanga na sasa Adolf Mtasingwa anaomba kuondoka! Azam kunabomoka, nyie hamuogopi?!

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post