Mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga SC, waimejikuta kwenye mgogoro wa uongozi kufuatia uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeamua kuwa uongozi wa sasa, ukiongozwa na Rais Eng. Hersi Said, sio halali. Hii ni baada ya kesi iliyofunguliwa mwaka jana na wanachama wawili wa Yanga SC, Juma Magoma na Geofrey Mwaipopo.
Kesi ya Magoma na Mwaipopo ilihusu
uhalali wa Katiba ya 2020 iliyotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022
uliomweka madarakani Engineer Hersi. Walisema kuwa katiba hiyo haikuwa halali
hivyo wakapinga utumizi wake katika uchaguzi. Ushindi wao katika kesi hiyo
mwezi Agosti 2023 ulikuwa hatua muhimu kufikia kufichua ukiukwaji katika mabadiliko ya uongozi.
Uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama kwa
upande wa kundi la Wazee wa Yanga unazidi kuimarisha haja ya mabadiliko ya
uongozi. Uamuzi wa mahakama unakubaliana na uhalali wa Katiba ya 2011, ambayo
wazee wanadai ndiyo ilikuwa halali na ilipaswa kutumika wakati wa uchaguzi huo
wanaougomea. Hukumu hii kwa ujumla wake inatia shaka msingi mzima wa urais wa
Engineer Hersi na uhalali wa utawala wake.
Uamuzi wa mahakama umewaacha wanachama na
wapenzi wa Yanga SC katika hali tete. Uongozi wa sasa ukiongozwa na Rais
Engineer Hersi Said, sio halali, swali la nani atachukua hatamu linabaki bila
jibu. Uamuzi huo unafungua njia ya kurudi kwa Katiba ya 2011, ambayo inaelekeza
Mkutano Mkuu unaowashirikisha wanachama wote, sio wawakilishi wa matawi tu,
kama mfumo wa sasa unavyotaka. Mkutano huu Mkuu ndiyo ungesimamia uchaguzi mpya
ili kuunda muundo halali wa uongozi.
Vita vya uongozi vinavyoendelea vinaweka
matatani mustakabali mzima wa Yanga SC. Ukosefu wa utulivu unaweza kuathiri ari
ya wachezaji, mahusiano na wadhamini, na shughuli za jumla za klabu.
Mashabiki wa Yanga SC kote Tanzania na kwingineko bila shaka wanatamani ufumbuzi wa haraka kwa mgogoro huu wa uongozi. Uwazi na kufuata katiba ya klabu ni muhimu kurejesha utulivu na kuhakikisha Yanga SC inaweza kuendeleza utawala wake katika soka la Tanzania, na katika kuhakikisha hilo linatokea klabu hiyo imeitisha mkutano na waandishi wa habari leo tarehe 17 Julai saa nane mchana kutolea ufafanuzi suala hio.
Na Luck Mwaifuge
Post a Comment