Kutoka Viti vya VIP Hadi Selo za Polisi: Makamu wa Raisi wa Shirikisho la Soka la Colombia Akamatwa Baada ya Fainali ya Copa America

Usiku wa mchezo wa fainalii ya Copa America uliozikutanisha timu za Argentina na Colombia, uliomalizika kwa Argentina kushinda goli 1-0, ulitazamiwa kuwa usiku wa sherehe ya soka Amerika Kusini. Hata hivyo, mchezo huu mzuri uligubikwa na vurugu za mashabiki kabla ya mechi na tukio la kushangaza baada ya mechi lilomshirikisha afisa wa juu wa soka.

Ramon Jesurun

Mapema Jumatatu asubuhi, makamu wa raisi wa Shirikisho la Soka la Colombia (CONMEBOL) Ramon Jesurun, alikamatwa kwa mashtaka ya kumpiga mlinzi wa usalama katika mechi hiyo ya fainali. Kulingana na ripoti, mzozo huo ulitokea mbele ya vyombo vya habari baadae. Jesurun, pamoja na mtoto wake Ramon Jamil Jesurun, inadaiwa waliagizwa kurudi nyuma na maafisa wa usalama ambapo wao walikaidi na hatimaye kuingia kwenye mapigano ya kimwili na mlinzi huyo.

Kukamatwa kwa vigogo hao kunaongeza mzozo mwingine kwenye fainali ya Copa America ambayo tayari iligubikwa na vurugu za mashabiki kabla ya mchezo wenyewe. Polisi wa Miami waliwakamata watu kadhaa nje ya Uwanja wa Hard Rock wakati mashabiki wasio na tiketi wakijaribu kuingia kwa nguvu uwanjani. Suala la mechi muhimu ya fainali katika mashindano ya Copa America kugubikwa na vurugu za mashabiki na kukamatwa kwa kiongozi wa juu wa soka kwa kosa la jinai kunaleta taswira isiyependeza katika mchezo wa soka.

Siku ya kusikilizwa mashtaka ya Jesurun inatazamiwa kufuatiliwa kwa karibu na jumuiya ya soka ya Colombia na duniani kote. Tukio hili linaleta maswali kuhusu mwenendo ndani ya vyombo vya uongozi wa mchezo huu. Je, maafisa wa soka waliokabidhiwa dhamana ya kuongoza mashirikisho ya soka ni waadilifu kwa kiasi gani?

Usiku wa fainali ya Copa America ulitakiwa kuwa usiosahaulika katika soka la Amerika Kusini, lakini kwa bahati mbaya utakumbukwa kwa sababu zisizofaa. Uzuri wa mechi yenyewe ulizuiliwa na  msisimko kutokana na vurugu zilizotokea nje ya uwanja na kuharibu ladha na sifa za mchezo huu mzuri.

Post a Comment

Previous Post Next Post