Enzo Fernandez |
Chini ya meneja mpya, Enzo Maresca, maandalizi ya msimu mpya wa Chelsea yalitazamiwa kuwa mtiririko wa mazoezi na
mbinu bora kuashiria mwanzo wa zama mpya kwa klabu hiyo. Badala yake, video
iliyosambaa mtandaoni ikimuonyesha kiungo Enzo Fernandez imeiingiza klabu hiyo
katika mzozo usiotarajiwa.
Video hiyo, iliyorekodiwa wakati wa
sherehe za ushindi wa Argentina kwenye Copa America, inamuonesha Fernandez
akiimba wimbo unaochukuliwa na watu wengi kuwa "wa ubaguzi". Miongoni
mwa watu waliokerwa na video hiyo ni mchezaji mwenzake wa Chelsea Wesley
Fofana. Tukio hili la Fernandez limewasha moto wa hasira, na kufanya Chelsea
kujitahidi kudhibiti mwelekeo wa habari hiyo na kudumisha taswira yao kama
klabu ambayo imejengwa juu ya misingi ya uwajibikaji.
Wachezaji wa Argentina walisikika
wakiimba wimbo ufuatao katika video iliyorekodiwa na Fernández, “Wanaichezea Ufaransa, lakini wanatoka
Angola. Mama yake ni Mnigeria, baba yake ni Mkameruni. Lakini kwenye pasipoti:
Mfaransa”. Wachezaji wa Chelsea wanaoichezea timu ya taifa ya Ufaransa
wanaonekana kukerwa sana na kiungo huyo wa zamani wa Benfica. Klabu ya
Chelsea ina kundi kubwa la wachezaji wa
Ufaransa wenye asili ya Afrika wakiwemo Malo Gusto, Lesley Ugochukwu,
Christopher Nkunku, Wesley Fofana, Axel Disasi na Benoït Badiashille.
The
Blues walijibu kwa haraka wakitoa lawama kali dhidi ya
video hiyo. "Klabu ya Chelsea haikubaliani na aina zote za tabia za
ubaguzi," ilisema taarifa hiyo. Zaidi walisisitiza zaidi nia yao ya
uwajibikishwaji na kuthibitisha kuanzishwa kwa hatua za kinidhamu za ndani
dhidi ya Fernandez.
Fernandez, aliyekuwa na furaha ya ushindi
wa Copa America, tayari ameomba msamaha akionesha majuto kwa matendo yake,
akidai maana ya wimbo huo "haihusiani na tabia au imani zake." Hata
hivyo, kuomba msamaha huenda kusiwe na nguvu ya kuzima moto wa mzozo huu.
Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF)
limeapa kuchukua hatua za kisheria kuhusiana na suala hilo, hatua ambayo
inaweza kuhatarisha hali ya kazi yake kimataifa. “Kwa kuzingatia ukubwa wa
matamshi haya ya kutisha, ambayo yanapingana na thamani za michezo na haki za
binadamu, rais wa FFF ameamua kuwasiliana moja kwa moja na mwenzake wa
Argentina na FIFA ili kuwasilisha malalamiko ya kisheria kwa sababu ya matamshi
ya kibaguzi," shirika la mpira wa miguu la Ufaransa limesema katika
taarifa yake. Taarifa hiyo iliongeza kuwa rais wa FFF Philippe Diallo
"anakemea vikali matamshi yasiyokubalika ya kibaguzi yaliyotolewa dhidi ya
wachezaji wa timu ya Ufaransa kama sehemu ya wimbo ulioimbwa na wachezaji na
wafuasi wa timu ya Argentina." Wakati huo huo, uchunguzi wa ndani wa
Chelsea unazidi kuwa mkubwa, huku uwezekano wa adhabu ukimngoja kiungo huyo.
Kadiri msimu mpya unavyokaribia, uwepo wa Enzo Fernadez katika klabu ya Chelsea unazidi kutokuwa wa uhakika. Je, atakabiliwa na adhabu kubwa? Wachezaji wenzake watamchukuliaje atakaporudi? Tukio hili limesababisha giza zito juu ya kile kilichotakiwa kuwa kipindi cha kusherehekea kati ya Chelsea, Fernandez na wachezaji wengine.
Post a Comment