Kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Soka Uingereza - EPL - klabu ya Chelsea maarufu kama The Blues imetambulisha jezi mpya itakazozitumia katika mechi zake za nyumbani msimu huu wa 2024/2025.
Klabu hiyo yenye maskani yake jijini
London imetoa taarifa ya jezi hizo kupitia kurasa zake za kijamii na kuashiria
mwanzo wa zama mpya kwa timu hiyo. “Msimu mpya. Zama mpya. Moto mpya”
yalisomeka maelezo ya taarifa hiyo na kuongeza “Tunatambulisha jezi ya nyumbani
ya Chelsea kwa msimu wa 2024/25.”
Kama kawaida rangi kuu katika jezi hiyo
ya nyumbani ya Chelsea ni bluu ikinakshiwa na alama zenye kuonesha miale ya
moto inayofanana na madoadoa ya mafuta ikiwa ni ishara ya malengo ya timu
kufanya vizuri ndani na nje ya uwanja.
Jezi mpya ya Chelsea inakuja kipindi
ambacho timu hiyo inakaribisha mameneja wapya, Enzo Maresca kwa kikosi cha
wanaume, na Sonia Bompasfor kwa kikosi cha wanawake.
Jezi hizo zilizotambulishwa msimu huu
hazina nembo ya mbele ya mdhamini kama ilivyokuwa kwa za msimu uliopita na
Chelsea bado wanatafuta mdhamini mpya mara baada ya mkataba wao wa msimu mmoja
na Infinite Athlete kumalizika. “Jezi zetu mpya tayari zinapatikana duniani
kote japo hazina nembo ya mbele ya mdhamini. Iwapo tutapata mdhamini siku
zijazo, mashabiki wataweza kupata aina hizo za jezi kwa kununua katika duka
letu na mtandaoni. Bahati mbaya hatutoweza kuwabadilishia jezi hizo kwa mpya
zenye nembo”, Ilisema taarifa ya klabu hiyo.
Wakati mzuka wa jezi mpya ukiwa bado haujapoa, Chelsea tayari wameshaanza maandalizi ya kuanza msimu ujao wa 2024/25 chini ya Maresca na Bompastor. Timu ya wanaume tayari imeshaanza kambi na inajiandaa kwa ziara nchini Marekani.
Post a Comment