Donny van de Beek Kujitafutia Girona

Klabu ya Girona iliyopanda daraja kushiriki Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, imethibitisha kumsajili kiungo wa Uholanzi Donny van de Beek kutoka Manchester United kwa ada ya usajili €500,000. Van de Beek ambaye aliwahi kutazamiwa kuwa mchezaji mwenye kipaji kikubwa na kutumainiwa kuja kufanya makubwa na mashabiki wa Manchester United amepitia kipindi kigumu cha kuporomoka kwa kiwango chake hali iliyopelekea kukosa nafasi katika kikosi cha Mashetani hao Wekundu na sasa anaanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka akitazamia kurejesha kiwango kilichomfanya kuwa nyota hapo awali.

Donny Van de Beek

Van de Beek alisajiliwa na Manchester United mwaka 2020 kutoka Ajax Amsterdam, uhamisho ambao ulipokelewa kwa shangwe nyingi na mashabiki wa United kwani alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Ajax ambapo alikuwa na mchango mkubwa katika utawala wao wa ligi ya ndani na pia aliwasaidia kuingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya 2018/19.

Van de Beek alitarajiwa kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha United. Hata hivyo, mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa. Chini ya Ole Gunnar Solskjaer na mrithi wake Erik ten Hag, van de Beek alishindwa kupata muda wa kucheza mara kwa mara hali iliyopelekea mara kadhaa atolewe kwa mkopo kwenda timu za Everton na Eintracht Frankfurt ambako napo alishindwa kuonesha mabadiliko makubwa, huku majeraha yakizuia zaidi maendeleo yake.

Girona kupanda ligi kuu ya La Liga ni fursa kwa Van de Beek kujitafuta upya. Wakali hawa wa Catalunya wanafahamika kwa kucheza soka safi la kushambulia kwa kasi kutumia washambuliaji na viungo wao na hii itatoa fursa kwa kiungo huyo kuonesha uwezo wake kama akipata nafasi. Uwezo wake wa kutawala mchezo hususani eneo la katikati la uwanja, kupanga mashambulizi, na kuunganisha wachezaji wenzake unalingana kabisa na falsafa ya Girona.

Akiwa na umri wa miaka 27, van de Beek bado ana uwezo mkubwa na nafasi ya kurudi kwenye kiwango chake bora kama akipata mfumo ambao utaendana na uwezo wake wa kiufundi.

Kuwasili kwa Van de Beek pia kunatazamiwa kuleta chachu mpya katika kikosi kichanga cha Girona. Uzoefu wake alioupata katika timu kubwa kama Ajax na Manchester United, licha ya kupata muda mchache wa kucheza, utamuwezesha kuwaongoza wachezaji wenzie ndani na nje ya uwanja.

Kwa Girona, usajili wa van de Beek ni kama kamari. Ingawaje hajawa na kiwango bora hivi karibunii, kipaji chake na uwezo wake sio vitu unavyoweza kuvikataa. Ikiwa akiweza kurudisha makali yake, anaweza kuwa mchezaji muhimu kwa Girona na kuwasaidia kuelekea kutawala kwenye La Liga.

Post a Comment

Previous Post Next Post