Hispania ni Dhababu Iliyopitishwa Kwenye Moto Kabla ya Kung'aa Hivi

Wanafainali wa mashindano ya Euro 2024, Hispania, wamewahi kutawala mpira wa miguu miaka kadha iiyopita. Washindi hao wa Kombe la Dunia mwaka 2010, na Kombe la Mataifa ya Ulaya 2008 na 2012 wamewahi kuwa na kikosi kilichowahi kuitwa cha dhahabu kikisheheni mafundi kama Villa na Iniesta.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Hispania walionekana kuwa na wakati mgumu katika mashindano ya kimataifa na hata ule ubora wao wa kupika vijana wadogo wenye vipaji vikubwa ulikwama. Mwaka 2014 walifurushwa katika Kombe la Dunia kwa kichapo cha aibu cha magoli 5-1 kutoka kwa Uholanzi. Hawakufanya vizuri pia kwenye Kombe la Mataifa Ulaya 2016 na Kombe la Dunia 2018.

Hata hivyo, katikati ya changamoto zote hizo bado kuna tumaini lipo. Shirikisho la Mpira Hispania wanaamua kucheza kamari kwa kutokutafuta kocha mwenye jina kubwa katika soka la Ulaya na badala yake timu anakabidhiwa mtu ambaye amekuwa akifanya kazi za kuzalisha na kukuza vipaji vya vijana nchini Hispania, Luis de la Fuente. Fuente sio kocha mwenye jina kubwa Ulaya kama ilivyokua kwa watangulizi wake, lakini anawafahamu vizuri wachezaji wa Hispania kuliko hao makocha wengine.

Siku za mwanzo Luis de la Fuente hazikuwa na dalili nzuri kwani mwaka jana walipokea kipigo cha magoli 2-0 kutoka kwa Scotland, matokeo yaliyoibua mijadala juu ya uwezo wa kocha huyo. Lakini Shirikiso la Mpira Hispania lilibaki na msimamo wake wa kumuamini kocha wao, imani ambayo hivi sasa inawalipa. Ukiwaangalia Hispania wakicheza utapata taswira halisi ya uwezo wa De la Fuente, soka safi la umiliki wa mpira na pasi nyingi fupi fupi huku wakishambulia kwa kasi.

Hispania wana wachezaji hatari kama vile Pedri, Lamine Yamal na Nico Williams, lakini mafanikio ya timu yao hadi kufika hatua ya fainali ya mashindano ya Euro 2024 sio matokeo ya uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, au wawili bali timu nzima. Tofauti na timu kama Uingereza ambao mara kadhaa wamekuwa wakimtegemea mchezaji mmoja aamue mechi, au Ufaransa ambao walimtegemea sana Kylian Mbappe. Hispania wao wanacheza kitimu na hakuna mchezaji mmoja aliye juu ya wengine.

Kikosi cha Hispania Euro 2024

Umoja huu ndio uliowafanya Hispania wafanye vizuri katika mashindano ya Euro 2024 kwanza kwa kuongoza katika kundi lao, huku wakifanikiwa kuzifunga timu ngumu kama vile Italia, Ujerumani na Ufaransa.

Swali lililobaki kwao ni iwapo wataweza kuendeleza ubora walionao sasa, Je, wataweza kupambana na Uingereza katika mechi ya fainali hapo Jumapili? Majibu ya maswali haya tutayapata katika dimba la Berlin hapo Jumapili. Hata hivyo bila kujalisha matokeo yatakuwaje katika mchezo wao wa fainali, safari ya Hispania inatoa funzo kubwa sana kuhusu uvumilivu, kuhusu umoja katika timu badala ya kutegemea mtu mmoja mmoja. Hadithi ya Hispania sio tu kuhusu kufika fainali; bali kuhusu namna walivyopambana kutoka kwenye hali ngumu waliyokuwa nayo miaka ya katikati mpaka kurudi kuwa miongoni mwa timu bora duniani.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post