Lamine Yamal Hawazi Kufananishwa na Messi

Mchezaji nyota wa Hispania, Lamine Yamal, kwa mara ya kwanza amezungumzia picha inayovuma mtandaoni ikimuonesha yeye akiwa mtoto mchanga akiogeshwa na Lionel Messi.

Lionel Messi Akimuogesha Lamine Yamal

Licha ya picha hiyo kuibua minong'ono ya kulinganishwa kwa wachezaji hao, Yamal amesema wazo lake kuu ni juu ya mechi ya fainali ya Euro 2024 kati ya timu yake dhidi ya Uingereza na kuwaasa mashabiki waache kumlinganisha na gwiji huyo.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 16, ambaye amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Hispania kwenye mashindano haya amezungumzia picha hiyo ambayo ilipigwa mwaka 2008 katika tukio la hisani la klabu ya Barcelona ambapo inamuonesha kinda huyo akiogeshwa na gwiji wa Barcelona wakati huo, Lionel Messi.

Licha ya kupata mafanikio makubwa kwenye mashindano ya Euro ikiwemo kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga katika historia ya mashindano hayo, Lamine Yamal amekiri kumheshimu Lionel Messi na na kwamba kamwe hawezi kuwa kama yeye bali nae ana njia yake binafsi. 
”Hakuna asiependa kulinganishwa na watu bora zaidi” alisema, “Lakini siwezi kuwa yeye. Nina njia yangu binafsi. Ukinilinganisha na Messi ni jambo la kustaajabisha. Vyombo vya habari vinataka tu kupata mchezaji wa kumlinganisha na Messi tena. Hili linanisumbua wakati mwingine. Nilikuwa nikimwangalia mazoezini na kutamani kuchezea kikosi cha kwanza kutimiza ndoto yangu na kucheza pamoja naye, kwa bahati mbaya Messi ni Idol na sijioni ninastahili kulinganishwa naye, na ninatumai tu kufikia nusu ya alichokifanya, bila shaka ni bora zaidi katika historia.”
Naye mchezaji wa zamani wa Uingereza, Garry Lineker, amekosoa tabia ya wachambuzi na watangazaji wa soka kuwalinganisha wachezaji hao akisema, "Ni makosa sana kumlinganisha Lamine Yamal na Wachezaji wakubwa kwa sababu umri wake bado mdogo sana, Hata Lionel Messi alikuwa baadae siwezi kusema atakuwa kama Messi au Maradona lakini tu anaweza kuja kufanya kile anachoweza kwa umri wake.”

Timu ya taifa ya Hispania inatarajia kukutana na Uingereza katika mchezo wa fainali wa mashindano ya Euro 2024 na lengo kubwa la Yamal ni kuisaidia nchi yake kushinda mchezo huo na sio kuwazia kulinganishwa kwake na gwiji huyo wa Argentina.

Hadithi ya kusisimua ya mafanikio ya Lamine Yamal haiishii tu katika soka. Siku chache zilizopita alifanikiwa kufaulu mitihani yake ya 4 ya ESO kuonesha kwamba yuko vizuri sio uwanjani tu bali hata darasani.

Nyota huyu wa Hispania mwenye thamani ya € milioni 90 na mkataba na Barcelona mpaka mwaka 2026 anatumainiwa kufanya vizuri katika safari yake ya soka sio tu na mashabiki wa mpira bali hadi wachezaji wenzie kama vile Ollie Watkins wa Uingereza aliediriki kusema kwamba Yamal ana kipaji cha pekee, maoni ambayo yameungwa mkono wa mashabiki wengi.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post