Enzo Fernandez Atarejea Chelsea Licha ya Tuhuma za Ubaguzi wa Rangi

 

Enzo Fernandez

Kiungo wa kati wa Chelsea, Enzo Fernandez anatarajiwa kurejea mazoezini Jumatatu baada ya changamoto inayomkabili juu ya tuhuma zinazomhusisha katika uimbaji wa wimbo wenye viashiria vya ubaguzi wa rangi. Mchezaji huyo mwenye miaka 23 alionekana kwenye video akiimba wimbo uliotafsiriwa kuwa dharau na kejeli dhidi ya wachezaji wa Ufaransa wenye asili ya Afrika baada ya Argentina kushinda Kombe la Amerika Kusini.

Tukio hilo ambalo limelaaniwa sana na mchezaji mwenzake, Wesley Fofana, huku akielezea video hiyo kuwa ni "ubaguzi wa rangi". Shirikisho la Soka la Ufaransa pia limeonyesha mshtuko wake kuhusu wimbo huo.

Tayari Fernandez ameomba msamaha kwa wachezaji wenzake wa Chelsea, ambao sita kati yao ni Wafaransa wenye asili ya Afrika, na pia hadharani, huku klabu ikianzisha taratibu za kinidhamu dhidi yake. Shirikisho la soka duniani FIFA pia limeanzisha uchunguzi wake kuhusu suala hilo.

Mchezaji mwenzake wa Chelsea, Noni Madueke, amesema kuwa suala hilo litatatuliwa ndani ya kikosi, na kocha Enzo Maresca ameonyesha uhakika kwamba suala hilo litapatiwa ufumbuzi ndani ya kikosi.

Nahodha Reece James ameonyesha utayari wake wa kuwa mpatanishi miongoni mwa wachezaji wenzake kama akilazimika kufanya hivyo, huku Chelsea wakiendelea na mfululizo wao wa mechi za kujiandaa na msimu mpya nchini Marekani, huku wakicheza na timu kama Celtic, Club America, Manchester City na Real Madrid.

Wakati suala la Fernandez linatia doa klabu, Chelsea wanatarajia kuweka mjadala huo nyuma na kuzingatia kujenga timu kwa ajili ya msimu ujao huku wakiweka nguvu kubwa katika kuzoea mtindo wa soka wa Maresca, ambao ni tofauti na ule wa kocha wa zamani Mauricio Pochettino.

Post a Comment

Previous Post Next Post