Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Hispania Wakishangilia Kunyanyua Kombe La Euro 2024 |
‘It is Coming Home’ itaendelea kuwa ndoto isiyotimia kwa waingereza tangu mwaka 1966 - waliposhinda Kombe la Dunia dhidi ya Ujerumani Magharibi - mara baada ya mchezo wa fainali ya mashindano hayo kutamatika pale katika dimba la Berlin kwa Hispania kupata ushindi wa magoli 2-1 na hivyo kuhitimisha msimu wao bora kabisa wa mashindano haya.
Fainali hii ilikuwa ni vita dhidi ya mitindo tofauti ya uchezaji: Uingereza walicheza kwa namna ya kujilinda muda mwingi huku Hispania wakishambulia wakati wote. Kwa mbinu hizo, Uingereza walifanikiwa kujilinda kipindi cha kwanza cha mchezo kupelekea timu zote ziende mapumziko zikiwa hazijafungana goli hata moja, kipindi cha pili kikawa na mabadiliko ya kimbinu kutoka kwa kocha wa Hispania, Luis de la Fuente. Dakia 45 za kipindi cha pili cha mchezo huo zilishuhudia Hispania wakiongeza kasi ya kushambulia hali iliyowasaidia kupata magoli mawili na hivyo kushinda.
Ushindi wa Hispania katika mechi hii ya fainali haujawa kitu cha kushangaza kwani ni kitu ambacho wengi walikitarajia kulingana na namna ambavyo wamekuwa wakicheza mechi zao kwa kushambulia kwa kasi wakiwatumia mawinga wao vijana, Nico Williams na Lamine Yamal, aina ya uchezaji ambayo kwa namna ambavyo Uingereza wanacheza kamwe wasingeimudu.
Kabla mchezo wa fainali, Hispania walikuwa wamezifunga timu zote 6 walizokutana nazo, na kati ya timu hizo kuna Croatia, Italia (waliokuwa mabingwa watetezi), wenyeji Ujerumani pamoja na Ufaransa wakati huo Uingereza walikuwa wanahangaika kupata matokeo kwa timu kama Slovakia, Slovania na Denmark!
Lamine Yamal na Nico Williams ndio walioshirikiana kuwapatia Hispania goli la uongozi, goli lililofungwa na Williams aliepokea pasi safi kutoka kwa Yamal. Uwezo walionao wachezaji hawa, namna wanavyocheza kwa kuelewana na kutokuchoka watimizapo majukumu yao uwanjani inatoa taswira nzima ya namna ambavyo bado timu hiyo ina muda mrefu sana wa kuendelea kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Matarajio ya nahodha wa Uingereza, Harry Kane, kubeba taji imekuwa mzigo mzito kwake kuubeba. Ndani ya miaka 14 ya Kane kucheza soka amefanikiwa kucheza michezo 643, fainali 6 huku akiwa hajabeba kombe hata moja! Katika mchezo huu, Kane alitolewa dakika ya 60 timu yake ikiwa inaongozwa goli, dakika chache tu baada ya yeye kutoka Uingereza wakasawazisha kupitia kwa Cole Palmer.
Kocha wa Uingereza, Gareth Southgate, ambae hatosahaulika kwa kufika fainali mbili za Euro bila kushinda yoyote, ataendelea kukosolewa na mashabiki wa soka kwa mbinu zake za kizamani za kujilinda sana na tabia yake ya kuchelewa kufanya mabadiliko yanayohitajika kwenye mchezo. Katika mchezo huu wa fainali, mbinu ya Uingereza kujilinda iliwasaidia kipindi cha kwanza lakini kushindwa kwao kuendana na kasi ya kushambulia ya Hispania kukawafanya wapoteze mchezo. Kipigo hiki kitaibua maswali katika kibarua cha meneja huyo iwapo atafaa kuendelea kufundisha kikosi cha Uingereza.
Kocha wa Hispania, Luis de la Duente, kwa upande mwingine anatazamwa kama shujaa alieweza kuwanoa na kuwatumia vizuri wachezaji wake kama vile Nico Williams, Lamine Yamal, Mikel Oyarzabal, Dani Olmo na wengineo. Luis de la Fuente, ambaye uteuzi wa yeye kuwa kocha wa Hispania uliibua minong'ono na ukosoaji mwingi, amewazima midomo wale waliombeza. Alionesha imani kwa vijana wenye vipaji huku akitumia mbinu ya kushambulia kwa ujasiri, na kuwangoza Hispania kushinda mechi zote katika Euro 2024.
Katika hatua nyingine, ndoto ya nyota wa Uingereza, Jude Bellingham kubeba tuzo ya Ballon d'Or huenda ikawa imefikia kikomo baada ya Uingereza kupoteza mchezo wa fainali. Tuzo ambayo hivi sasa kuna uwezekano mkubwa ikachukuliwa na nyota wa Hispania, Rodri, ambaye pia ametangazwa kuwa mchezaji bora wa mashindano ya Euro 2024.
Na Luck Mwaifuge
Post a Comment