Kipa wa Manchester City aliyeisaidia timu hiyo kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, Ederson, anakabiliwa na maamuzi magumu katika maisha yake ya soka. Kipa huyu fundi kutoka Brazil amekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya Pep Guardiola pale City, uwezo wake wa kuokoa michomo mikali ukiwa na mchango mkubwa katika utawala wa City. Hata hivyo, ofa nono kutoka kwa mtajiri wa mafuta wa Saudi Arabia inaweza kumuondoa Uingereza.
Ederson Santana de Moraes |
Klabu ya Al-Nassr, inayojulikana kwa mikakati yao ya kuvutia wachezaji wakubwa, inadaiwa kutoa ofa kubwa sana kwa ajili ya huduma ya Ederson. Wanapanga kumpa mshahara wa pauni 900,000 kwa wiki, pamoja na bonasi kubwa ya usajili! Kiwango hiki kikubwa cha pesa kutoka uarabuni hakilingani na mshahara kiduchu wa sasa wa Ederson hali inayoweza kumfanya afikirie kumtimkia Al Nassr. Pamoja na hilo, Ederson anaweza kutaka kwenda kujiunga na Cristiano Ronaldo huko Mashariki ya Kati, ambapo nyota huyo wa Ureno anafurahia maisha yake ya mwishoni ya soka.
Wakikabiliwa na uwezekano wa kumpoteza kipa wao muhimu, Manchester City wanajitahidi kumbakisha nyota huyo pale Etihad. Wakati wakikubaliana na uhalisia kwamba hawawezi kushindana kifedha na ofa ya matajiri hao wa Saudia, City wako tayari kutoa ofa yenye maboresho ya kimkataba kwa Ederson ikiwa ni pamoja na ongezeko la asilimia 75 la mshahara wake wa sasa unaokadiriwa kuwa pauni milioni 1 kwa mwezi. Ofa hii ni msisitizo wa nia ya City kumbakisha Ederson, ikitambua mchango wake mkubwa kwenye mafanikio yao.
Kwa mazingira hayo, maamuzi ya iwapo ataipa kipaumbele heshima na ushindani wa Ligi Kuu ya Uingereza, ambapo amejizolea sifa kuwa mmoja wa makipa bora duniani Au fedha na maisha mazuri zaidi nchini Saudi Arabia ni juu ya Ederson mwenyewe.
Mkataba wa sasa wa Ederson utakwisha miaka miwili ijayo, hivyo City wanataka kuhakikisha wanamuongezea mkataba mapema sana badala ya kuchelewa. Ukweli ni kwamba hawatoweza kumlazimisha kipa huyo kubaki iwapo yeye hatotaka hivyo ada ya uhamisho ni kitu cha muhimu kwao kuzingatia ili washawishi. Ikiwa Ederson ataamua kuondoka, City wanatarajiwa kudai ada ya pauni milioni 50, pesa nyingi ambayo inaweza kuwekezwa tena katika kuimarisha sehemu nyingine za kikosi.
Kwa sasa Ederson anafurahia mapumziko mara baada Brazil kutolewa mapema katika mashindano ya Copa America. Nyota huyo anatarajiwa kurejea Uingereza baadaye mwezi huu kujumuika na Manchester City katika ziara yao ya maandalizi huko Marekani. Macho na masikio yote yatakuwa kwa kipa huyo ataamua kitu gani kuhusu maisha yake ya baadaye. Je, ataendelea kusalia katika klabu iliyomfikisha hapo alipo, na kuendelea kuimarisha ukuta wa City kwa miaka mingine ijayo? Au atashawishiwa na utajiri unaotolewa na Al Nassr?
Na Luck Mwaifuge
Post a Comment