Euro 2024: Watkins Aibeba Uingereza Kuwafuata Hispania Fainali

Olie Watkins Akishangilia Goli la Ushindi dhidi ya Uholanzi

Ni rasmi sasa Uingereza wamejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya fainali ya mashindano ya Euro kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuwaondosha mashindanoni Uholanzi kwa ushindi wa magoli 2 kwa 1 walioupata jana Jumatano, shukrani kwa goli la dakika za jioni la Olie Watkins alieingia kipindi cha pili katika mechi hiyo akitokea benchi. Kwa matokeo hayo, Uingereza wanawafuata Hispania katika hatua ya fainali ya mashindano hayo, mechi itayochezwa siku ya Jumapili katika dimba la Olympiastadion Berlin.


Macho na masikio yote ya wapenzi wa soka nchini Uingereza yalikuwa jijini Dortmund wakati vijana wa Gareth Southgate, ambao ni washindi wa pili wa mashindano ya Euro yaliyopita, wakijaribu kutengeneza historia nyingine, kazi ambayo haikuwa rahisi na iliwalazimu kutoka jasho kweli kweli kuwazuia Xavi Simons, Memphis Depay na wachezaji wengine wa Uholanzi.

Uholanzi ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli mnamo dakika ya 7 tu ya mchezo kupitia kwa Xavi Simons. Hata hivyo kuruhusu goli dakika za mwanzoni za mchezo haikuwafanya Uingereza wakate tamaa na hatimaye dakika ya 18 tu wakasawazisha kwa mkwaju wa penati kupitia Harry Kane na hivyo kipindi cha kwanza kuisha kwa sare ya 1-1.

Pengine, kwa maoni ya wengi, hii ndiyo mechi bora zaidi kuchezwa na Uingereza katika mashindano haya kwa mwaka huu kwani wamekuwa wakikosolewa vikali kwa namna yao ya kucheza katika mechi zilizopita. Hii ni mechi ambayo Uingereza wameshuhudiwa wakimiliki mpira sana na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Phil Foden, ambaye mara nyingi amecheza mbavu ya kushoto alikuwa tishio kwa pasi zake kuelekea langoni kwa Uholanzi na amewanyanyasa vilivyo.

Baada ya kusawazishiwa, Uholanzi hawakupoa na wamewapa Uingereza changamoto hivyo kuhakikisha wapenzi wa soka duniani kote wanashuhudia mechi ya hadhi ya Nusu Fainali.

Kipindi cha pili cha mechi hii kilishuhudia kutambulishwa mchezoni nyota wa Uholanzi, Wout Weghorst ambaye alileta utulivu eneo la katikati hali iliyowafanya Uingereza wazidishe nidhamu ya kujilinda.

Wakati kila mmoja akiwa amekubali kwamba mechi itaenda dakika 30 za nyongeza, Southgate anaamua kuiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji kwa kuwaingiza uwanjani Cole Palmer na Watkins kuwabadili Phil Foden na Hary Kane, mabadiliko ambayo yanamlipa kwa asilimia zote. Sekunde za mwishoni za mchezo, Cole Palmer anapiga pasi murua inayomkuta Watkins ndani ya boksi la Uholanzi ambaye nae hafanyi makosa anatumbukiza mpira nyavuni.

Ushindi huu wa dakika za jioni wa Uingereza sio tu kwamba unawafanya wacheze fainali kwa mara ya pili mfululizo, lakini pia unawaandikia Uingereza rekodi muhimu. Kikosi hiki cha mwaka huu ndio kikosi cha kwanza cha Uingereza kufika hatua ya fainali wakiwa ugenini. Lakini pia, hivi sasa wanayo nafasi ya kuandika historia nyingine kwa kushinda kombe la Euro kwa mara ya kwanza na kizingiti pekee kilichopo mbele yao ni Hispania ambao watakabiliana nao siku ya Jumapili katika mechi ya fainali.

Ikumbukwe kwamba, Hispania ndiyo timu ambayo inashikilia rekodi ya kuchukua kombe hili mara nyingi -mara 3- na hawajawahi kupoteza mchezo wowote wa fainali.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post