Yanga na Azam Zawajua Wapinzani Wao Klabu Bingwa Afrika

 


Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika yani mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga SC, na washindi wa pili wa ligi hiyo, Azam FC wanarejea katika mashindano haya na tayari wameshapangiwa wapinzani watakaokutana nao.

Kwa mujibu wa droo ya Ligi ya Mabingwa msimu huu iliyochezeshwa alasiri, Julai 11, Yanga watamenyana na Vital’O ya Burundi huku Azam wao wakijiandaa kuwakabili APR ya Rwanda katika hatua ya awali ya mashindano hayo.

Je, Yanga Wataendeleza Walipoishia Msimu Uliopita?

Wananchi katika msimu uliopita wa mashindano haya - 2023/2024 - walifanikiwa kufika hatua ya robo fainali ambapo walitolewa na Mamelodi Sundowns kwa changamoto ya mikwaju ya penati. Ni matumaini ya mashabiki wa timu hiyo na wapenzi wa soka nchi nzima kwamba watafanya vizuri zaidi msimu huu ingawaje sio rahisi kama ambavyo inaweza kudhaniwa.


Wapinzani wa Yanga katika hatua ya awali ya mashindano haya ni Vital'O FC wa Burundi ambao hawatarajiwi kuwapa urahisi Wananchi kupenya kwenda hatua inayofuata ambapo mshindi kati yao atakutana na mshindi wa mechi kati ya SC Villa ya Uganda dhidi ya Commercial Bank ya Ethiopia.

Ili kuhakikisha kwamba msimu huu wanafanya vizuri zaidi, Yanga tayari wamefanya maboresho mengi katika kikosi chao ikiwemo kuwasajili kiungo Clatous Chota Chama kutoka Simba SC na mshambuliaji Prince Dube kutoka Azam FC.


Azam FC: Usajili Mpya Utaleta Tumaini Jipya?

Wawakilishi wengine wa Tanzania katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu ni Azam FC kutoka Chamazi, ambao wanajaribu bahati yao kuweza kufuzu kwenda hatua ya makundi ya mashindano hayo, hatua ambayo hawajawahi kuifikia.

Hata hivyo njia ya Azam FC kuelekea makundi sio rahisi kwani wanatarajiwa kuanza kampeni yao kwa kuwakaribisha mabingwa wa Rwanda, APR FC na kisha mshindi wa jumla kati yao ataenda kukutana na mshindi wa jumla kati ya JKU ya Zanzibar na Pyramids FC.

Katika kuhakikisha wanakuwa na msimu bora Azam FC wamefanya maboresho kadhaa katika kikosi chao ikiwa ni pamoja na kusajili wachezaji katika nafasi mbalimbali ikiwemo beki wa kati Yoro Diaby, mshambuliaji Jhonir Blanco, kiungo mshambuliaji Franck Tiesse, kiungo mkabaji Ever Meza na wengineo.

Matarajio ya wapenzi wa soka nchini ni kuona timu hizi zikifanya vizuri katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika msimu huu na ushindi kwao ni ushindi kwa taifa zima.

Yanga, ambao wana uzoefu katika mashindano ya kimataifa na kikosi imara wanatazamiwa kufanya vizuri zaidi. Je, watafanikiwa kufika hatua ya makundi na hatimaye kufika mbali zaidi ya walipoishia msimu wa 2023/2024? Azam FC kwa upande mwingine, wanayo nafasi ya kuandika upya hadithi yao katika soka la Afrika. Je, watafanikiwa kufika hatua ya makundi na kujitengenezea jina katika soka la Afrika? Wiki chache zijazo zitatupa majibu ya maswali haya na mengine mengi.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post