Euro 2024: Wenyeji Ujerumani Wafurushwa Mashindanoni

Goli la dakika za mwisho za kipindi cha pili cha dakika 30 za nyongeza, zikiwa zimebaki sekunde 65 tu mechi iende kuamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati, la Mikel Merino linawapatia Hispania ushindi wa magoli 2-1 na kuwahakikishia nafasi ya kucheza hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Euro 2024 na kuwafurusha wenyeji, Ujerumani.


Hispania walipata goli la uongozi katika mchezo huu dakika ya 51 ya mchezo kupitia nyota wao Dani Olmo aliyepokea pasi murua kutoka kwa kinda wa Barcelona Lamine Yamal. Goli la kusawazisha la Ujerumani lilifungwa dakika ya 89 na Florian Wirtz hivyo kufanya dakika 90 zitamatike kwa sare ya goli 1-1 na kupelekea mechi iende dakika 30 za ziada.

Katika hatua ya Nusu Fainali, Hispania watakutana na Ufaransa ambao wamefanikiwa kutinga hatua hiyo mara baada ya kuwaondoa mashindanoni Ureno kwa kuwabamiza penati 5-3.

Ujerumani wamekuwa na muendelezo mbovu katika mashindano makubwa ya kimataifa na kikosi cha mwaka huu kilibeba matumaini ya mashabiki wa soka nchini humo kwamba angalau kinaweza kufanya makubwa, ndoto iliyoyeyuka baada ya kuondoshwa katika hatua ya Robo Fainali.

Toni Kroos, kwa ubora na uzoefu alionao, pengine alitazamiwa na Hispania kuwa mchezaji hatari zaidi wa Ujerumani kabla ya mechi hiyo, lakini tunaweza kusema ndiye aliekuja kuwasafishia njia ya ushindi baada ya kumchezea rafu Pedri dakika ya 7 tu ya mchezo na hivyo kusababisha Pedri atolewe nje nafasi yake ikichukuliwa na Dani Olmo aliekuja kubadili kabisa sura nzima ya mchezo kwa kufunga goli ya uongozi la Hispania dakika ya 51 huku akitoa pasi ya mwisho kwa mfungaji wa bao la ushindi, Merino, dakika ya 119!

Toni Kroos Akimchezea Faulo Pedri

Mashindano ya Euro 2024 yanatarajiwa kuendelea tena leo, Julai 6 kwa michezo miwili ya hatua ya robo fainali kupigwa; Katika mchezo wa kwanza Uingereza watakutana na Uswisi ndani ya dimba la Merkur Spiel-Arena huku kivumbi kingie kikipigwa katika dimba la Olympiastation kuwakutanisha wababe wawili Uholanzi na Uturuki.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post