Kwa mshambuliaji nyota wa Ujerumani na Arsenal, Kai Havertz, maisha yamekuwa matamu zaidi. Hii ni baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Sophia Weber, na sasa Havertz yuko tayari kusahau kuhusu machungu ya kukosa Kombe la Euro 2024 akiwa na timu yake ya taifa ya Ujerumani na kuanza msimu mpya wenye matumaini ya ushindi na klabu yake ya Arsenal huku akiwa na mpenzi wa maisha yake.
Ingawa safari ya Ujerumani kwenye Euro
2024 ilimalizika kwa namna ya kusikitisha kwani waliishia katika hatua ya robo
fainali, Havertz amepata faraja baada ya sherehe ya ndoa yake na Weber mnamo
Julai 18. Katika picha nzuri kutoka kwenye sherehe hiyo zilizopakiwa kwenye
mtandao maarufu wa Instagram, wanandoa hao walitangaza upendo wao kwa maneno
machache lakini yenye nguvu: "18.07.24
- milele."
Kai Harvetz na mke wake Sophia Weber |
Msimu uliopita ulikuwa msimu bora sana
kwa Havertz, katika maisha binafsi na kwenye soka, kwani: Alisajiliwa kutoka
Chelsea kwenda Arsenal na kisha kuingia haraka katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo akijihakikishia kuwa mchezaji
muhimu katika kikosi cha washika mtutu hao wa jiji la London. Msimu wake wa
kwanza ulikuwa wa kuvutia kwani alifanikiwa kupachika mabao 14 na kutoa pasi 7
za usaidizi katika mechi 51 kwenye mashindano yote. Havertz aliendeleza kiwango
chake kizuri hadi katika Euro 2024 akiwa na Ujerumani akifunga mabao mawili na
kutoa pasi moja ya usaidizi katika mechi tano!
Sherehe za harusi zikiisha, Havertz
anatarajiwa kuungana tena na kikosi cha Arsenal wiki ijayo. Washika Mtutu hao
wa jiji la London wanafanya ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya nchini
Marekani, ambapo wakiwa huko wanatarajia kukabiliana na baadhi ya majina
makubwa ya Ulaya, ikiwa ni pamoja na Manchester United, Liverpool na Bayer
Leverkusen. Ziara hii inayosubiriwa kwa hamu itakuwa mtihani muhimu kwa Havertz
na wenzake wanapojengeana uelewano zaidi na kuboresha mikakati chini ya meneja
wao Mikel Arteta.
Kwa mwelekeo mpya, mke wa kumuunga mkono, na ziara ya maandalizi ya msimu mpya ili kuboresha uwezo wake, Havertz anaonekana kuwa tayari kwa kuanza msimu mzuri na Arsenal. Je, ataweza kurudia rekodi yake ya kuvutia ya ufungaji na kuwaongoza Arsenal kwenye mbio za ubingwa wa Uingereza msimu ujao wa 2024/2025? Mashabiki wa Arsenal kote duniani watatazamia kwa karibu kumuona Havertz mpya uwanjani na nje ya uwanja.
Post a Comment