Mexico Kutafuta Kocha Mpya Baada ya Lozano Kubwaga Manyanga

Mustakabali wa soka la Mexico umegubikwa na sintofahamu baada ya kuondoka kwa meneja Jaime Lozano. Kocha huyo aliteuliwa mwaka 2023 na kisha kushinda michuano ya  CONCACAF Gold Cup, uongozi wa Lozano katika timu hiyo uliingia doa baada ya kuonesha kutokufanya vizuri kwenye Copa America.

Jaime Lozano

Timu hiyo ya taifa ya Mexico, maarufu kama El Tri, iliondoshwa katika mashindano ya Copa America 2024 hatua ya makundi ikifanikiwa kushinda mchezo mmoja tu dhidi ya Jamaica huku ikipokea kipigo kutoka kwa Venezuela na kupata sare dhidi ya Ecuador, matokeo yaliyoonesha mapungufu katika mbinu za kocha huyo licha ya kuwa na kikosi chenye wachezaji wazuri.

Katika kuhakikisha hawafanyi vibaya kuelekea Kombe la Dunia 2026, Shirikisho la Mpira la Mexico (FMF) lilijaribu kumpa Lozano ofa ya mkataba mpya wenye masharti lakini ameitupilia mbali. Ofa hiyo ilimtaka Lozano kubaki kuwa kocha msaidizi chini ya meneja mwenye uzoefu zaidi hadi Kombe la Dunia la 2026, mashindano ambayo Mexico inataka sana kushiriki. Baada ya Kombe la Dunia, Lozano angerejeshwa tena nafasi ya kocha mkuu, akiiongoza timu hiyo katika kipindi kilichobaki. Hata hivyo, Lozano alikataa pendekezo hilo.

“Jaime Lozano na benchi lake lote walipewa ofa ya kubaki na sisi mpaka 2030, ambapo kati ya mwaka 2024-2026 katika kampeni yetu ya Kombe la Dunia wote watamsaidia kocha mkuu mwenye uzoefu zaidi,” Shirikisho hilo lilisema katika taarifa yake, “na baadae itakuwa ni Lozano mwenyewe atakayechukua nafasi ya kocha mkuu kuanzia 2026 mpaka 2030. Baada ya kuipitia ofa yetu, kocha huyo amesema asingependa kuendelea na sisi tunaheshimu uamuzi wake.”

Hali hii inawaacha FMF wakitafuta kocha mpya wakati huu ambapo Kombe la Dunia la 2026 linakaribia huku ikiwa kuna shinikizo la kupata mtu sahihi kuwaongoza El Tri kufuzu na uwezekano wa kuingia katika mashindano yenyewe. Ripoti zinasema kwamba Javier Aguirre, ambaye aliiongoza Mexico kwenye Kombe la Dunia la 2002 na lile la 2010, ndiye anayetazamiwa kuja kuchukua nafasi hiyo.

Je, Aguirre, au mtu yeyote atakayekuwa kocha, ataweza kuwafikisha El Tri katika fainali za Kombe la Dunia 2026? Wakati pekee ndio utaweza kutuambia ukweli, lakini jambo moja ni hakika: mustakabali wa soka la Mexico uko mikononi mwa FMF na utafutaji wa meneja sahihi ni hatua muhimu kuelekea kurejesha nafasi yao miongoni mwa timu bora duniani.


Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post