Mchezo wa Ligi ya Norway, Eliteserien, wa jana Jumapili kati ya Rosenborg na Lillestrom uliahirishwa kutokana na vurugu za mashabiki waliokuwa wakipinga matumizi ya teknolojia ya VAR.
Dakika 30 za mwanzo za mechi hiyo
zilishuhudia matukio ya kushangaza kutoka kwa mashabiki wa timu zote mbili
ambao waliungana katika kutokubaliana kwao na VAR, walirusha mvua ya vitu
mbalimbali uwanjani ikiwa ni pamoja na mipira ya tenisi na mikate huku wakisababaisha
milipuko ya baruti.
Mashabiki wa Rosenborg, wanaojulikana kwa
ushangiliaji wao wa vurugu, ndio waliofanya kitendo cha kwanza cha upinzani.
Walirusha mipira ya tenisi uwanjani na kisha wenzao wa Lillestroem wakawaunga
mkono hali iliyopelekea waamuzi kusitisha mchezo. Katika kuhakikisha mamlaka
husika zinapata ujumbe wao, mashabiki hao hawakuishia tu kufanya vurugu lakini
pia walitandaza bango lililotangaza
kupinga kwao teknolojia ya VAR: "Hatutakata tamaa kamwe, VAR itaondoka!"
Licha ya onyo kali kutoka kwa mtoa
matangazo wa uwanjani kwamba kuendelea kwa vurugu zaidi kungesababisha
kuahirishwa kwa mchezo huo, vurugu za mashabiki hao hazikuweza kuzimwa. Mipira
zaidi ya tenisi iliendelea kutupwa uwanjani kuonesha uthabiti wa nia yao
waliendelea kuimba “Tunachukia, tunachukia VAR, Tunachukia, tunachukia
VAR” na ujumbe wao ulikuwa wazi: VAR
haitakiwi. Hatimaye mwamuzi hakuwa na budi kusitisha mchezo huo kabisa.
Kuahirishwa kwa mchezo wa Rosenborg na
Lillestrom kunakumbushia juu ya malalamiko ya mashabiki wa mpira wa miguu kote
duniani kuhusu VAR. Wakati malengo ya teknolojia hii ni kuhakikisha usahihi wa
maamuzi uwanjani, inaonekana kuwa inaathiri radha na mtiririko mzima wa mchezo.
Post a Comment