Simba SC na Elie Mpanzu Ngoma Ngumu

Katika dirisha hili kubwa la usajili, klabu ya soka ya Simba imefanya mabadiliko kadhaa katika kikosi chake ikiwa ni pamoja na kuacha na kusajili wachezaji mbalimbali. Katika kuhakikisha wanaboresha safu yao ya ushambuliaji, moja ya mchezaji aliyekuwa katika rada zao ni winga machachari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Elie Mpanzu. Kwa ubora alionao uwanjani, uwezo wa kumiliki mpira, kasi ya ukokotaji mpira na uwezo wake wa kufunga na kupiga pasi za mwisho za magoli, Mpanzu alionekana kuwa kipande kinachokosekana katika jitihada za Simba kutawala soka la Afrika. Lakini jitihada za wababe hawa kumjumuisha katika kikosi chao msimu huu hazijafanikiwa kuzaa matunda.

Elie Mpanzu

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 ni miongoni wa wachezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha AS Vita cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwa sababu hiyo haijawa rahisi kwa waajiri wake hao kumuachia aondoke kikosini. Simba, ambao msimu huu wanatarajiwa kushiriki katika Kombe ya Shirikisho la CAF wapo katika harakati za kufanya kila linalowezekana kufanya vizuri katika mashindano hayo na kumleta Mpanzu kikosini ilikuwa ni mpango mojawapo katika jitihada hizo.

Winga huyo ambaye alitazamiwa kuwa angeweza kuwavuka mabeki wa wapinzani wa Simba kwa ustadi na kupiga krosi murua ambazo zingewanufaisha washambuliaji wa Simba alishaanza kufanya mazungumzo na klabu ya hiyo na ilionekana kwamba ni suala la muda tu kabla mchezaji huyo hajatambulishwa katika viunga vya Msimbazi, lakini sasa mambo yameenda ndivyo sivyo.

Ripoti zinaarifu kwamba Mpanzu yeye alikuwa tayari kuwatumikia Simba SC, na katika harakati hizo  aliwapotosha maafisa wa Simba kwa kuwaaminisha kwamba hana mkataba na AS Vita lakini AS Vita wamethibitisha kwamba wana mkataba wa mwaka mmoja na mchezaji huyo hivyo njia sahihi kwa Simba kumpata ilikuwa ni kuongea nao na sio kuongea na mchezaji moja kwa moja. Mazungumzo, ambayo hapo awali yalikuwa na matumaini, yakageuka kuwa wimbo wa huzuni.

Hata hivyo Simba walikuwa na nia ya dhati kumsajili nyota huyo, na katika kuthibitisha hilo maofisa wa Simba wamefanya mazungumzo na uongozi wa AS Vita mara 3 ili kuwashawishi lakini katika kuhakikisha hilo halitimii AS Vita, ambao sasa wapo chini ya ufadhili wa wawekezaji wa Kituruki, walitaka pesa nyingi - $250,000 - ili kumwachia winga huyo. Ada hii kubwa iligeuka kuwa pigo la mwisho katika harakati za Simba kumsajili Mpanzu katika dirisha hili.

Dirisha la usajili linapoelekea kufungwa, Simba SC wanajikuta wanarudi kwenye hatua ya kwanza tena. Jitihada zao za kupata winga mbunifu bado hazijafikiwa, na kuacha pengo kubwa katika mipango yao ya kushambulia. Mashabiki ambao hapo mwanzo walifurahia uwezekano wa kuwasili kwa Mpanzu, sasa wamebaki na wimbo wa kukata tamaa.

Hata hivyo, bado kuna nafasi. Simba bado wana chaguo la kumfuata tena Mpanzu mwezi Januari dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa tena. Zaidi ya hayo wameamua kumrudisha kundini kiungo wao Willy Esomba Onana hali ambayo inatoa matumaini kidogo. Onana, japo siyo mchezaji mzuri kama alivyo Mpanzu, bado anaweza kuwasaidia katika eneo la ushambuliaji kama alivyofanya msimu uliopita.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post