Yanga SC Kukiwasha Kombe la Mpumalanga la Afrika Kusini!

Mashabiki na wadau wa mchezo wa mpira wa miguu, Tanzania, bado hawajausahau msimu bora wa 2023/24 wa Yanga. Young Africans Sports Club, au Wananchi kama wanavyojulikana na mashabiki wao, walikuwa na msimu bora sana. Vikombe vya kutosha kwenye kabati lao - taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara maarufu kama Kombe la NBC, na ushindi wa Kombe la Shirikisho la (FA) yakiwa kama ishara ya utawala wao katika soka la ndani, huku katika mashindano ya kimataifa wakifanikiwa kufika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika. Wakati wanapoendelea kujiandaa na msimu ujao, changamoto mpya inawangoja - Kombe la Kimataifa la Mpumalanga nchini Afrika Kusini.

Mashindano haya ya kabla ya msimu, yanatarajiwa kuanza leo Julai 20 hadi Julai 27, yatawapa Yanga nafasi ya kujaribu uwezo wao katika ardhi ya kigeni kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa 2024/25. Mechi ya ufunguzi tu yenyewe inatarajiwa kuwa mechi bora kuwahi kutokea katika historia ya klabu hii, ikiwakutanisha mabingwa hao wa Tanzania na wababe wa Bundesliga ya Ujerumani, FC Augsburg.

Mechi hii ina umuhimu mkubwa kwa pande zote mbili: kwa Yanga, ni nafasi yao kuonesha ubabe wao nje ya mipaka ya Tanzania. Huku kwa FC Augsburg, hii ni mara yao ya kwanza kuweka kambi ya maandalizi ya msimu nje ya Ulaya hivyo watataka kuona ni kitu gani cha tofauti wanaweza kukifanya.

Kwa aina ya kikosi walichonacho, ni dhahiri kwamba, Yanga wataingia uwanjani wakiwa hawana hofu ya kukabiliana na wababe hao wa Ujerumani. Wakiwa wamefanikiwa kubaki na kikosi chao cha kwanza kilichowawezesha kufikia mafaniko makubwa msimu uliopita, na namna ambavyo wameimarika kwa kufanya makubwa kwenye usajili, wanacho kikosi kilichojaa vipaji na uzoefu wa kutosha kuwapa changamoto FC Augsburg. 

Mashindano haya yatatumika kama fursa kwao kutumia na kuboresha mbinu zao, kuingiza wachezaji wapya kwenye mfumo uliopo, na muhimu zaidi, kuonyesha ubora wao wa kimbinu katika ulimwengu wa soka wa Afrika.

Ratiba ya Yanga katika Kombe la Mpumalanga:



Julai 20: Yanga SC vs FC Augsburg (4:00 AM EAT)

Julai 27: Mchezo wa mtoano (mpinzani na muda kutangazwa baadae)

Kombe la Mpumalanga ni hatua ya kwanza ya Yanga kuuelekea msimu mpya wa 2024/2025 ili kuona kama wataweza kukidhi haja za wapenzi wao ikiwa ni pamoja na:

● Kutetea taji lao la Ligi Kuu ya Tanzania

● Kutetea taji la Kombe la Shirikisho la (FA)

● Kufanya vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa ya CAF - kufika hatua ya mbele zaidi katika mashindano hayo (nusu fainali)

Kwa kikosi kilichosheheni wachezaji wenye vipaji vikubwa, mwalimu mwenye mbinu na ujuzi wa kutosha na mashabiki wanaowapa ‘sapoti’ kila wakati, Yanga SC wanatarajiwa kufanya vizuri katika mashindano hayo na msimu mzima wa 2024/2025. Ushiriki wao katika Kombe la Mpumalanga unatazamiwa kuwa ni mwanzo mzuri kuelekea msimu mpya.

Post a Comment

Previous Post Next Post