YAMETIMIA: Rasmi Clatous Chama Ni Mwananchi

Klabu ya Yanga imetangaza kukamilishi dili la kumvuta Jangwani nyota wa kimataifa wa Zambia, fundi Clatous Chota Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea kwa watani wao wa jadi Simba Sports Club.

Clatous Chota Chama Akisaini Yanga

Chama ameondoka Simba kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na timu hiyo kutamatika tarehe 30 Juni 2024 na kwa mantiki hiyo basi Simba hawajapata kiasi chochote cha pesa katika dili hilo.

Klabu ya Yanga imekuwa ikifukuzia saini ya mchezaji huyo kwa zaidi ya misimu miwili tangu alipoondoka RS Berkane ya Morocco na hatimaye yametimia katika dirisha hili la usajiri.

Clatous Chota Chama anaondoka Simba huku akiacha manung'uniko kwa mashabiki wa timu hiyo kwani alikuwa mchezaji wao pendwa na ni matamanio ya wanachama na mashabiki wengi wa timu hiyo kuwa Chama angeendelea kuwa mchezaji wa Simba.

Isisahaulike kwamba Simba ndiyo waliomtambulisha Chama katika soka la Tanzania baada ya kumsajili mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya nchini kwao Zambia kabla ya kumuuza kwenda RS Berkane msimu wa 2020/2021 ambapo aliwatumikia kwa miezi 6 tu kabla hajarejea tena Simba alikodumu mpaka sasa anasajiliwa kwenda Yanga.

Clatous Chama anawapa mkono wa kwa heri Simba akiwa amewatumikia katika jumla ya michezo 179 huku akiwafungia magoli 42 na kutoa pasi za magoli 60 hivyo ameondoka akiwa bado ni mchezaji muhimu katika kikosi hicho.

Mpaka sasa Yanga wameshafanya sajili za wachezaji Prince Dube na Clatous Chama huku kikosini wakiwa tayari na wakali kama Yao Kwasi Atoula, Max Nzengeli, Azizi Ki, Pacome Zouzou, Aucho na wengineo na dirisha la usajili ndio kwanza limefunguliwa. Yanga kuna mchoro wanauchora, TUNAOGOPA!

Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post