Yanga Watawala Tuzo za TFF 2023/24

Tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) za msimu wa 2023/24 zimefanyika usiku wa kuamkia leo huku klabu ya Yanga ikithibitisha ufalme wake katika ushindani wa soka la ndani.

Kiungo Stephan Azizi Ki, alikuwa nyota wa wa usiku wa tuzo hizo za TFF. Uwezo wake wa kufunga mabao ulimpatia tuzo ya mfungaji bora, huku ujuzi wake katika eneo la kiungo ukimpatia tuzo ya Kiungo Bora. Ilikuwa sherehe murua kwa mashabiki wa Yanga kwani kipa wao, Djigui Diarra, alipata tuzo ya kipa bora, uthibitisho wa uimara wa klabu hiyo katika soka la Tanzania.

Stephen Azizi Ki (Katikati) akipokea tuzo

Simba Queens, klabu inayoongoza kwa wanawake, pia ilikuwa na usiku mzuri na wa kukumbukwa kwani mchezaji wao Aisha Mnunka alijipatia tuzo za Mfungaji Bora na Mchezaji Bora hali iliyoakisi utawala wa Simba katika ligi ya wanawake.

Pamoja na kutawala kwa Yanga na Simba Queens kwenye ligi zao, tuzo zilitolewa pia kwa watu waliofanya vizuri katika maeneo mengine katika mchezo wa soka: Tuzo za kocha bora zilienda kwa Miguel Gamondi wa Yanga SC kwa ligi ya wanaume na Juma Mgunda wa Simba Queens kwa ligi ya wanawake.

Tuzo hizo zilitambua pia mafanikio ya wachezaji wa Tanzania wanaofanya makubwa kimataifa. Mbwana Samatta, anayekipiga katika klabu ya PAOK FC ya nchini Ugiriki, alipewa tuzo ya mchezaji bora wa kiume anayecheza nje. Vile vile, Aisha Masaka, anayesajiliwa na klabu ya Brighton nchini Uingereza alipewa tuzo ya mchezaji bora wa kike anayecheza nje.

Leodegar Tenga, rais wa zamani wa TFF, alipokea tuzo ya heshima kwa huduma yake kubwa katika mchezo wa soka nchini huku marehemu Said El Maamry, akitangazwa kutunukiwa tuzo ya heshima.

Tuzo za TFF za mwaka 2023/24 zimeonesha kutambua ukuaji na maendeleo ya soka la Tanzania. Klabu kama Yanga SC na Simba Queens zimeinua kiwango cha ligi, huku kutambuliwa kwa wachezaji wanaofanya vizuri nje ya nchi kukiwa ni ushahidi wa ongezeko la ushawishi wa vipaji vya Tanzania kimataifa.

Na Luck Mwaifuge

Post a Comment

Previous Post Next Post