Klabu ya Azam imemtangaza Rachid Taoussi kuwa kocha mkuu mpya kwa ajili ya kuimarisha benchi lao la ufundi. Kocha huyo kutoka Morocco amejiunga na Azam kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Taoussi, kocha mwenye uzoefu mkubwa katika soka la Afrika Kaskazini, anakuja na timu ya wasaidizi watatu: Ouajou Driss (kocha msaidizi), Badr Eddine (kocha wa utimamu wa mwili), na Rachid El Mekkaoui (kocha wa makipa). Usajili wa kocha huyu mpya katika viunga vya Chamazi unakuja siku chache baada ya matajiri hao kumfurusha aliyekuwa kocha wao mkuu, Yousouph Dabo, ambaye alitimuliwa kutokana na matokeo mabaya ya timu mwanzoni mwa msimu.
Taoussi, ambaye alikuwa kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Morocco, ana rekodi nzuri ya mafanikio, akiwa amefundisha vilabu kadhaa vikubwa katika nchi yake kama vile RSB Berkane, AS Far Rabat, Wydad Casablanca, na CR Belouizdad. Kuwasili kwake Azam FC ni hatua muhimu kwa Azam, kwani wanalenga kujiimarisha ili kuwa timu bora ndani na nje ya nchi.
Akiwa na Leseni ya UEFA Pro na uzoefu wa zaidi ya miongo miwili katika ukocha, Taoussi anatazamiwa kuja kuiongoza Azam FC kwa mafanikio makubwa. Uwezo wake wa kimbinu pamoja na uwezo wake wa kubadilika kulingana na mchezo husika vimemtengenezea sifa kama mmoja wa makocha bora katika ukanda wa Afrika Kaskazini.
Post a Comment