Baada ya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha magoli 900 katika mechi rasmi, Cristiano Ronaldo amefunga bao lake la 901 akiwafunga Scotland dakika za jioni kabisa na kuisaidia Ureno kuibuka na ushindi wa 2-1.
Mchezo huo, uliopigwa huko Ureno, ulikuwa mchezo wa kusisimua ambapo ilishuhudiwa Scotland ikipata goli la mapema kupitia nyota wake Scott McTominay aliefunga kwa kichwa. Licha ya kukabiliwa na shinikizo kutoka kwa washambuliaji wa Ureno, ulinzi wa Scotland ulibaki imara kwa kipindi kikubwa cha mchezo. Hata hivyo, hawakuweza kushikilia bomba kwa muda wote kwani dakika ya 54 tu ya mchezo, Ureno waliweza kusawazisha kupitia Bruno Fernandes.
Ronaldo alitambulishwa mchezoni mnamo kipindi cha pili cha mchezo akichukua nafasi ya Pedro Neto, mabadiliko yaliyo wabeba Ureno kwani dakika ya 88 ya mchezo, Ronaldo aliwafungia goli la ushindi akiunganisha mpira uliotoka kwa Nuno Mendes. Goli hilo liliongeza rekodi aliyoiweka juzi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha magoli 900 katika mechi rasmi, na sasa anayo 901!
Kufungwa kwa Scotland katika mechi hii kumeongeza rekodi yao mbaya ya kutokushinda, timu hiyo sasa imeenda michezo nane ya ushindani bila kupata ushindi, mfululizo mbaya zaidi katika historia yake.
Athari ya Ronaldo kwenye mchezo huo ilikuwa kitu kisichoweza kuepukika. Uzoefu wake, ujuzi, na nia yake thabiti ya kuhakikisha anaisaidia timu yake kila wakati vilithibitisha ndivyo vilivyodhihirisha tofauti kati ya timu hizo mbili.
Post a Comment