Katika kuhakikisha inaendelea kuboresha michezo, Serikali imeahidi kuongeza idadi ya viwanja vya michezo nchini, huku ikizielekeza mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga fedha kwa ajili ya jambo hilo.
Akizungumza bungeni jana, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), amesema lengo ni kuhakikisha kila wilaya ina angalau uwanja mmoja wa michezo.
“Tunataka kuona vijana wetu wanapata maeneo ya kufanya mazoezi na kukuza vipaji vyao vya michezo,” alisema Mwinjuma.
Mwinjuma ametoa mfano wa halmashauri kadhaa zilizopiga hatua katika ujenzi wa viwanja vya michezo, ikiwemo Kinondoni, Bukoba Mjini, Nyamagana, Namungo, Wang’ing’ombe, na Sengerema.
Kwa upande mwingine, Serikali inaendelea na ukarabati wa viwanja vikubwa vya Uhuru na Benjamin Mkapa, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Arusha. Viwanja vingine vitano vinakarabatiwa kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.
Mwinjuma amewataka viongozi wa mikoa na wilaya ambao mikoa na wilaya zao hazijajumuishwa katika miradi ya AFCON 2027 kuanza kujenga viwanja vya kisasa ili kuongeza vyanzo vya mapato katika maeneo yao.
Post a Comment