Beki wa Zamani wa Sheffield United, George Baldock, Afariki Dunia Akiwa na Miaka 31

 
George Baldock, mchezaji wa zamani wa Sheffield United na mchezaji wa kimataifa wa Ugiriki, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo akiwa na umri wa miaka 31. Mwili wa mchezaji huyo uliipatikana kwenye bwawa la kuogelea nyumbani kwake Glyfada, Athens.

Baldock alijiunga na klabu ya Panathinaikos ya Ugiriki hivi karibuni baada ya kuchezea Sheffield United kwa miaka 7, ambapo alijipatia umaarufu kwenye Ligi Kuu ya England.

Familia yake ililitaja tukio hilo kama mshtuko mkubwa kufuatia kifo hicho cha ghafla, wakisema, “Tuko katika mshtuko kutokana na suala hili kubwa.” Klabu ya Panathinaikos pia ilionyesha huzuni, ikielezea habari hizo kama pigo kubwa kwa klabu na jamii ya mpira wa miguu.

Sheffield United ikitoa salamu zake za rambirambi kwa familia na marafiki wa Baldock ilimsifu kama mchezaji mashuhuri miongoni mwa wachezaji wenzake, mashabiki, na wafanyakazi wakati wa kipindi chake kikosini mwao.

Baldock alicheza mechi 219 na Sheffield United na alikuwa na mchango mkubwa katika kupandisha timu hiyo hadi Ligi Kuu ya England mwaka 2019 na tena mwaka 2023.

Baldock aliichezea timu ya taifa ya Ugiriki Mei 2022 na jumla alipata nafasi ya kuiwakilisha timu hiyo mara 12, huku mchezo wake wa mwisho ukiwa Machi 2023. Shirikisho la Soka la Ugiriki lilielezea huzuni yao, wakisema, “Hakuna maneno ya kuelezea maumivu ya kupoteza mmoja kati yetu kwa namna ambayo hatukutarajia.”

Kifo cha Baldock kimeiacha jamii ya soka ya Ugiriki, na duniani kote, katika majonzi. Inaripotiwa kuwa mke wake alikuwa akimtafuta kwa saa kadhaa kabla ya mwili wake kugunduliwa. Uchunguzi wa mwili utafanywa siku chache zijazo, lakini polisi wameashiria kuwa hakuna dalili za mchezo mchafu.

Rambirambi zimekuwa zikimiminika kutoka pande mbalimbali katika ulimwengu wa soka. Harry Maguire, mchezaji wa zamani wa Sheffield United, na Dean Henderson walitoa ujumbe wa hisia, huku klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya England pia zikitoa pole zao.

Baldock alianza safari yake ya soka katika klabu ya MK Dons, na alikuwa na vipindi vya mkopo katika klabu mbalimbali kabla ya kujiunga na Sheffield United mwaka 2017. Ameacha alama ya kudumu ndani na nje ya uwanja, na kifo chake cha ghafla kimeiacha dunia ya soka ikiwa na huzuni kubwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post