Meneja wa zamani wa Liverpool, Jürgen Klopp, ameteuliwa kuwa mkuu wa soka wa makampuni ya Red Bull. Kocha huyo wa Kijerumani, ambaye aliongoza Liverpool kushinda mataji mengi makubwa, atachukua jukumu hili jipya kuanzia Januari 1, 2025.
Licha ya kustaafu ukocha, Klopp anataka kuendelea kuutumikia mchezo huo anaoupenda zaidi na anaona nafasi hii kama njia nzuri ya kuendelee kuunganishwa nao.
Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram, Klopp, 57, alithibitisha kwamba bado hajavutiwa kurudi kwenye benchi, lakini ana hamu ya kuchukua changamoto hii mpya.
“Bado napenda soka, na napenda kufanya kazi. Red Bull inanipa jukwaa zuri la kuendelea kuchangia kwenye mchezo ninaoupenda.”
Kampuni ya vinywaji ya Red Bull inashiriki sana katika ulimwengu wa michezo, ikimiliki vilabu vya soka kama vile RB Leipzig, Red Bull Salzburg, New York Red Bulls, na Red Bull Bragantino. Pia wana hisa katika klabu ya Leeds United ya Uingereza.
Klopp hatashiriki moja kwa moja katika shughuli za kila siku za timu hizi lakini atatoa mwongozo katika maeneo muhimu kama vile kuwaelekeza makocha, kusaidia kuendeleza vipaji na pia mikakati ya uhamisho katika timu zote za Red Bull.
“Nataka kushiriki uzoefu nilioupata kwa miaka mingi,” Klopp alisema. “Nimepigania kupandisha timu daraja, mataji, na tuzo. Wakati mwingine nimefanikiwa, wakati mwingine nimefeli, lakini kujifunza jinsi ya kushughulika na kazi zote hizi mbili ni sehemu ya safari.”
Klopp, ambaye aliacha jukumu lake la ukocha ndani ya Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita, alifurahia mafanikio makubwa wakati wake akiwa Anfield, akishinda Premier League, Ligi ya Mabingwa, na mataji mengine kadhaa. Kabla ya wakati wake huko England, alikuwa meneja wa Borussia Dortmund, ambapo alishinda mataji mawili ya Bundesliga na kufikia fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2013.
Mkurugenzi mtendaji wa miradi ya kampuni na uwekezaji wa Red Bull, Oliver Mintzlaff, alisifu ushawishi wa Klopp kwenye ulimwengu wa soka. “Jürgen Klopp ni moja ya watu muhimu katika mchezo wa soka, na utaalam wake utaleta athari chanya kwenye biashara zetu za soka duniani.”
Post a Comment